Monday, 8 April 2013


Tunamkumbuka, kumuenzi vipi Edward Moringe Sokoine






“Tutakutana tena kwa kikao kijacho cha Bunge hapa Dodoma. Mimi ninasafiri kwa gari kwenda Dar es Salaam, nitapitia Morogoro, naamini tutaonana huko.” Edward Sokoine 


KWA UFUPI
Ni miaka 29 tangu alipofariki dunia mwanasiasa huyu kwa ajali mbaya ya gari iliyotokea kule Dumila mkoani Morogoro wakati kiongozi huyo akitokea Dodoma kwenye mkutano wa Bunge.
Ijumaa, Aprili 12 mwaka huu itakuwa siku ya kumbukumbu ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine.
Ni miaka 29 tangu alipofariki dunia mwanasiasa huyu kwa ajali mbaya ya gari iliyotokea kule Dumila mkoani Morogoro wakati kiongozi huyo akitokea Dodoma kwenye mkutano wa Bunge.
Watanzania wengi ambao walikuwapo miaka ile ya uhai wake wanakumbuka jinsi ambavyo Sokoine alivyokuwa kiongozi imara, thabiti na ambaye aliipenda nchi yake.
Yeye, ndiye kiongozi mwingine ambaye zaidi ya Mwalimu Julius Nyerere, aliyediriki kutaifisha mali ambazo zilikuwa zikimilikiwa na watu wachache huku wengi wakiendelea kuwa maskini.
Unaweza kujiuliza, miaka 29 imepita tangu Sokoine aiage dunia, je, ni nani kati ya viongozi wetu wa sasa ambaye amefanikiwa au hata kujaribu kuvaa viatu vyake katika suala la uadilifu, ambalo kwa sasa linaonekana kuipiga chenga nchi yetu?
Kitu kingine kikubwa ambacho wewe kama Mtanzania wa leo unachoweza kujiuliza ni wangapi kati yetu, sisi wa kizazi cha wa sasa ambao tunawaheshimu viongozi wetu au hata kuwaheshimu kama ilivyokuwa kwa zama za Sokoine?
Tujiulize, tunacho kikao cha Bunge kinachoendelea kule mjini Dodoma ambako kwa bahati nzuri ndiko waliko viongozi wetu karibu wote walioko madarakani na hata upinzani, je wanajiuliza wao wenyewe ni kwa jinsi gani wanavyomuenzi Sokoine?
Kama nchi, tunayo miaka miwili na zaidi kidogo, kwa wengine kati yetu wanafikiria uchaguzi mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani na tayari wachache kati yao wanafikiria na kuwaza jinsi ya kuwania nafasi hizi za juu za uongozi katika nchi yetu, je, wanajifunza nini kwake (Sokoine), ambaye unaweza kumwita mwanahalisi wa nchi aliyeipenda nchi yake kwa kiasi kile?